Beki wa kati wa Simba, Abdi Banda
amesimamishwa kucheza Ligi Kuu wakati akisubiri suala lake la kumpiga
ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla wakati akiwa hana mpira
kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Banda anadaiwa kufanya kitendo hicho
ambacho hakikuonwa na waamuzi katika mechi kati ya Kagera Sugar na Simba
iliyofanyika Aprili 2, 2017 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Pia Kamati ilibaini kuwa Banda alifanya
kitendo cha aina hiyo kwenye mechi kati ya Simba na Yanga iliyofanyika
Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, Klabu ya Kagera Sugar iliwasilisha
malalamiko dhidi ya kitendo cha beki wa Simba, Abdi Banda kumpiga ngumi
kiungo wao George Kavilla wakati akiwa hana mpira, na Mwamuzi wa mechi
hiyo kutochukua hatua yoyote.
Kadhalika Klabu ya Simba iliwasilisha
malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana
na timu ya Kagera Sugar kumchezesha mchezaji Mohamed Fakhi Gharib
wakati akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194
iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo,
imeahirisha shauri hilo hadi Alhamisi Aprili 13, 2017 kwa vile bado
inafuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo kabla ya kufanya
uamuzi.