Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe.
Paul Makonda leo amehojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge kuhusiana na tuhuma za kuingilia haki, uhuru na madaraka ya Bunge.
Mhe. Makonda aliwasili Bungeni
Dodoma majira ya saa nne asubuhi kuitikia wito wa Kamati hiyo uliotokana
na Azimio la Bunge lililotolewa na Bunge, Februari 8, 2017 katika
Kikao cha Nane cha Mkutano wa Sita wa Bunge ambapo amehojiwa na kamati hiyo kwa
muda wa masaa matatu kuhusu tuhuma zinazomkabili.
Katika kikao hicho, Bunge liliazimia
kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Makonda na Mkuu wa Mkoa wa Arumeru,
Mhe. Alexander Mnyeti kuitwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na
Madaraka ya Bunge baada ya Bunge ili kujibu tuhuma hizo.
Akizungumza mara baada ya Kamati hiyo
kumaliza kazi yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka
ya Bunge, Mhe. George Mkuchika alisema Kamati hiyo imekutana leo baada ya
kuagizwa na Mheshimiwa Spika wa Bunge kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge.
“Tumefanya kikao hiki cha Kamati baada
ya kuagizwa na Mhe. Spika kwa kuwa kwa Mujibu wa Kanuni zetu, Kamati hii
inakutana pale tu inapoagizwa na Spika wa Bunge,” alisema.
Alisema Mhe. Spika aliiagiza Kamati
hiyo imuite Mhe. Makonda mbele ya Kamati kufuatia azimio hilo la Bunge
lililopitishwa na Bunge Februari 8, ambapo pamoja na mambo mengine Mkuu
huyo wa Mkoa alitakiwa kufika mbele ya Kamati kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
Alisema kwa mujibu wa Azimio hilo, Mhe.
Makonda alidaiwa kutoa kauli kupitia Televisheni ya Clouds akidai kwamba
wabunge wanasinzia Bungeni jambo lililoonekana kwamba ni kudharau Bunge.
“Napenda kutoa taarifa kwamba Mhe.
Makonda leo amekuja mbele ya Kamati na ametupa ushirikiano mzuri, tumepokea
maelezo yake na Kamati imemaliza kazi yake,” alisema.
Alisema kama ilivyo utaratibu, Kamati
yake itakabidhi taarifa yake kwa Mhe. Spika kwa mujibu wa Kanuni ambapo Spika
ndiye atakaeamua namna ya kutoa raarifa kuhusu kazi ya Kamati hiyo.