Dodoma: Wanywaji wa Pombe za Viroba Waja na Mbinu Mpya.

Baada ya sekeseke la kupiga marufuku uuzaji na unywaji wa pombe kali
viroba, wanywaji wa pombe za viroba mjini Dodoma wamebuni mbinu mpya ya
kununua pombe hiyo iliyopigwa marufuku huku watumiaji hao wakiipa pombe
hiyo jina la maziwa mgando au nzela.
Maeneo yanakopatikana viroba kwa wingi katika mji huo ni stendi ya Mkoa
wa Dodoma na Jamatini ambapo wafanyabiashara humimina pombe hiyo katika
chupa za konyagi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mtanzania kwa siku kadhaa mjini hapo,
umeonyesha jinsi pombe hiyo inavyouzwa kwa shilingi 1,000 baada ya
kujazwa kwenye chupa kubwa za konyagi.
Mmoja wa wauzaji wa pombe hiyo ambaye hakutaka kuandikwa jina lake
gazetini, alisema biashara imekuwa ngumu na wao wanahitaji kupata fedha,
hivyo wameamua kuja na njia mpya ya kuuza viroba hivyo. “Tutafanyaje
ndugu yangu, maisha magumu, tumeweka viroba katika chupa kubwa za
konyagi na tunawapimia kwa kutumia kakikombe kadogo kama ka kahawa kwa
shilingi 1,000,” alisema mfanyabiashara huyo.
Aliongeza”Siwezi kuacha hii biashara, hapa ni stendi, wasafiri na
makondakta wengi ndio wateja wetu na natengeneza fedha za kutosha,
lakini sasa hivi nawauzia tu watu ninaowajua, kwani naogopa kukamatwa.”
Naye mmoja wa wanunuzi wa viroba hivyo, alisema baada ya Serikali kupiga
marufuku uuzwaji wa viroba hivyo, wameamua kubadili mwelekeo wa kununua
bidhaa hiyo ili kukwepa mkono wa Serikali.


