Rais wa Uganda,
Yoweri Museveni amemhakikishia Rais Magufuli kuwa yupo tayari kuweka
jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini
Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Rais
Museveni amesema hayo jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam wakati akiagana na mwenyeji wake
Rais Magufuli baada ya kumaliza ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku 2
hapa nchini na kurejea Uganda.
Rais
Museveni aliwasili nchini juzi asubuhi ambapo amefanya mazungumzo na
mwenyeji wake Rais Magufuli na jana ametembelea viwanda viwili
vinavyomilikiwa na kampuni ya mfanyabiashara wa Tanzania Bw. Said Salim
Bakhresa ambavyo ni kiwanda cha uzalishaji wa unga wa ngano kilichopo
Buguruni na kiwanda cha uzalishaji wa juisi kilichopo Vingunguti Jijini
Dar es Salaam.
Licha ya kuwekeza nchini Uganda Mfanyabiashara huyo pia amekuwa akipeleka bidhaa zake kwa wingi nchini Uganda.
Pamoja
na Mhe. Rais Magufuli viongozi wengine waliokuwepo wakati wa kumuaga
Mhe. Rais Museveni ni pamoja Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa na Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na
Usalama.