Swaziland Yapiga Marufuku Wanafunzi kufundishwa Somo la Dini ya Kiislamu Mashuleni.
SERIKALI nchini Swaziland imeziagiza shule zake kufundisha somo la dini
ya Kikristo pekee, hatua iliokosolewa na wadau mbalimbali kwa kuwa
haiheshimu dini nyengine.
Agizo hilo lilitolewa wiki iliyopita na Wizara ya Elimu nchini humo,
ambapo ilipita shuleni ikiwaagiza walimu wakuu wote kuhakikisha mtaala
hautaji dini nyingine zaidi ya Kikristo.
Sahid Matsebula, ambaye ni Muislamu anayefanya kazi msikitini karibu na
Mji Mkuu wa Mbabane, alinukuliwa akisema kwamba sera hiyo huenda ikazua
wasiwasi wa kidini katika ufalme huo.
''Serikali ina mpango gani kwa watoto wetu ambao si Wakristo? Ambao
licha ya kujifunza wakiwa nyumbani, mambo mengine wanapaswa wajifunze
wakiwa shuleni,” alisema.
Sera hiyo mpya imekuja baada ya raia kulalamika kuhusu wahamiaji wa Bara
la Asia na wale wa Kiislamu kwamba wamekuwa wakiingia nchini humo hatua
iliyolazimu Bunge kuunda kamati ya kuchunguza tukio hilo.
Wahamiaji wengine tayari wamerudishwa makwao na Waziri wa Biashara,
Jabulani Mabuza ameliambia Bunge kwamba wameanza kutunga sheria
itakayowazuia wahamiaji kuanzisha biashara nchini Swaziland.
Rais wa Baraza la Makanisa nchini humo, Stephen Masilela ameunga mkono mtaala huo mpya.
''Ukristo ndio msingi wa kujengwa kwa taifa hili,” alisema.
Hata hivyo, Taifa la Swaziland linaloongozwa na Mfalme Mswati wa tatu tangu mwaka 1986, lina idadi ndogo ya waumini wa Kiislamu.
Sera hiyo ya kufundisha dini ya Kikristo pekee shuleni, pia imekosolewa
na mwandishi Nomsa Mbuli wa gazeti la Times of Swaziland.
“Kinachoinua dini moja juu ya nyengine ni nini wakati ambapo Katiba inaagiza usawa wa kidini?” alihoji.


