Ufaransa: Maelfu ya watu washindwa kuwatembelea ndugu zao wakati huu wa Krismasi
Sikukuu ya Krismasi haikuwa nzuri sana kwa wasafiri nchini Ufaransa wakati mgomo wa usafiri ukiingia katika wiki ya nne, na kuharibu mipango ya maelfu ya watu waliokuwa wakitaka kusherehekea na ndugu zao.
Watu wengi wamehangaika katika dakika ya mwisho kutafuta njia mbadala wakati maandamano dhidi ya mageuzi ya pensheni yakishuhudia maelfu ya treni zikifutwa ama kucheleweshwa , na taksi, huduma za kusafiri na wenye magari na mashirika ya magari ya kukodi yakishindwa kujaza pengo la upungufu wa matreni.
Maelfu ya watu wamekosa huduma ya usafiri wakati huu wa sherehe za krismasi katika miji mingi nchini Ufaransa
Ni sehemu ndogo tu ya treni za mwendo kasi na treni zinazosafiri kati ya miji mikuu zilitembea katika mkesha wa sikukuu ya Krismasi na hata treni chache zaidi zilifanyakazi katika sikukuu yenyewe jana.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha DW, Vituo vikuu vya treni mjini Paris vilifungwa majira ya asubuhi ambapo huduma za kwenda maeneo ya mashambani zilipunguzwa na ni njia mbili tu kati ya 16 za treni , zile ambazo hazina dereva ndio zilikuwa zinafanyakazi.
Rais Emmanuel Macron alitoa wito wa suluhu wakati huu wa sikukuu , lakini majadiliano kati ya serikali na vyama vya wafanyakazi wiki iliyopita yalishindwa kupata msimamo wa pamoja
Wagomaji waapa
Na wagomaji waliapa kwamba hakutakuwa na kusimamisha mgomo wakati wa kipindi hiki cha sikukuu hadi pale maafisa watakapoondoa mipango ya kuunganisha mifumo 42 ya pensheni kuwa mmoja.