Breaking News

Serikali mkoani Mbeya yasitisha upimaji na utoaji wa hatimiliki katika vijiji vya Kapunga na Ukwavila.


Wiki chache baada ya ITV kuripoti mgogoro wa mpaka baina ya vijiji vya Kapunga na Ukwavila wilayani Mbarali,hatimaye serikali mkoani Mbeya imeagiza kusitisha mchakato wa aina yoyote wa upimaji na umilikishaji wa ardhi katika hilo ili kupisha wataalam kutafuta mpaka halisi wa vijiji hivyo kwa lengo la kumaliza mgogoro huo wa mpaka uliodumu kwa zaidi ya miaka kumi.

Kabla ya kutoa uamuzi huo, Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ametembelea eneo lenye mgogoro na kisha kufanya kutano wa pamoja na wananchi wa vijiji vyote viwili vya Kapunga na Ukwavila na kusikiliza hoja zao kuhusu mahali ulipo mpaka halisi wa vijiji hivyo na ndipo akaelezwa kuwa licha ya kuwepo kwa mgogoro wa mpaka kwenye vijiji hivyo,wataalam wa ardhi wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali wanaendelea kupima na kutoa hati miliki kwa baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa na uwezo wa kifedha.

Baada ya kusikiliza hoja za wananchi hao,Mkuu wa mkoa wa Mbeya,Amos Makalla akaamua kusitisha mchakato wowote wa kupima na kutoa hati miliki kwenye eneo linalogombaniwa na wananchi wa vijiji vya Kapunga na Ukwavila.

Aidha mkuu huyo wa mkoa wa Mbeya akaagiza wataalam wa ardhi kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji hivyo pamoja na baadhi ya wananchi kufuatilia na kutambua mpaka halisi wa vijiji hivyo ndani ya siku 14 na kwamba mpaka utakaowekwa na wataalam ndio utakaotambuliwa na kuheshimiwa na pande zote mbili.