WAZIRI MKUU ABAINI GYPSUM ZA NJE HAZITOZWI KODI, AAHIDI KUFUATILIA SUALA.
*Aahidi kufuatilia suala hilo, asema lazima zitozwe kodi kulinda soko la ndani *Apokea mchango wa sh. milioni moja kwa ajili ya waliopatwa na maafa Kagera
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atafuatilia ili ajue chanzo ni kwa nini bidhaa za gypsum zinazoagizwa kutoka nje ya nchi hazitozwi kodi.
Waziri
Mkuu ametoa ahadi hiyo jana jioni (Jumapili, Oktoba 2, 2016) wakati
akizungumza na watumishi na viongozi wa kiwanda cha Premalt Limited
kinachotengeneza unga wa gypsum (gypsum powder) aina ya Afri Bond mara baada ya kukagua kiwanda hicho kilichopo Zuzu nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Waziri Mkuu alisema: “Gypsum inayozalishwa Dodoma ina ubora kama ile inayozalishwa Mchinga, kule Lindi na hakuna gypsum yenye ubora kama huo hapa Afrika isipokuwa gypsum ya Tanzania.”
“Nilikuwa sielewi ni kwa nini gypsum ya
wenzetu ilikuwa inakimbiliwa, lakini sasa nimetambua; ilikuwa na bei
nafuu kwa sababu tumetoa kodi. Sasa hivi, hili jambo nalibeba, naenda
kulishughulikia”.
“Nimeangalia kwenye orodha niliyopewa katika madini yote nimekuta kodi ya gypsum ni asilimia sifuri. Ni lazima tuweke kodi ili tutengeneze soko zuri kwa gypsum inayozalishwa
hapa nchini. Ni lazima tuweke kodi kwenye madini yetu mengine kama
makaa ya mawe ili tutengeneze soko zuri,” alisema.
Alisema
wakazi wa Dodoma wamepata fursa kutokana na uwepo wa kiwanda kama hicho
kwani kiwanda kinahitaji mali ghafi kwa hiyo ni jukumu la wakazi wake
kuchangamkia fursa ya uchimbaji wa madini hayo.
“Natambua
kwamba Mkurugenzi wa kampuni hii ataleta mitambo mikubwa zaidi hivi
karibuni. Nendeni benki mkakope ili muweze kununua zana za kuchimbia
madini haya. Yeye ukishafikisha hapa, ananunua ili aanze kusaga na
kupata unga wa gypsum,” alisema.
Alitumia
fursa hiyo pia kumpongeza mmiliki wa kampuni ya STJ Enterprises, Bi.
Adella Nungu ambaye ni mmoja wa wajasiriamali wa Kitanzania wanaotumia gypsum kutoka Dodoma na kutengeneza mapambo mbalimbali ya kuezekea ndani ya nyumba. Bi. Nungu alikuwepo kiwandani hapo.
Bi. Nungu alisema anaponunua unga wa gypsum kutoka
Dodoma, kwa wastani anaweza kutengeneza bidhaa za tani 20 hadi 25 kwa
mwezi kutegemea na hali ya soko na oda kutoka kwa wateja wake
Mbali ya kutengeneza mapambo ya kuezekea, unga wa gypsum hutumika
pia kutengeneza ‘muhogo’ (Plaster of Paris-POP) unaotumika kuwafunga
wagonjwa waliovunjika mifupa kama sehemu ya matibabu yao.
Mapema,
akisoma risala kwa niaba ya uongozi wa kampuni ya Premalt Limited, Bw.
Mohammed Ameir Mbaraka alisema wamefanya utafiti na kubaini kuwa
makontena ya gypsum yenye tani zaidi ya 3,000 yanaingizwa nchini bila
kutozwa kodi.
“Tumegundua kuwa gypsum inayoingizwa
kutoka nje ya nchi ni miongoni mwa bidhaa ambazo hazitozwi kodi.
Serikali ikiruhusu hali hii iendelee, itaathiri ajira za watumishi hapa
kiwandani,” alisema.
Alisema
mawe ya madini ya jasi (gypsum) yanachimbwa katika kijiji cha Manda
wilayani Chamwino, kilichopo umbali wa km. 80 kutoka Dodoma mjini.
Naye
Mwenyekiti wa kijiji cha Manda, Bw. Kambona Pius Matonya alimweleza
Waziri Mkuu kwamba kijiji hicho kina wakazi zaidi ya 300 ambao wengi wao
wanajishughulisha na uchimbaji wa madini hayo lakini wanakabiliwa na
changamoto ya ukosefu wa soko.
“Kijiji
chetu kipo katika jimbo la Mtera. Asilimia kubwa ya wakazi wanafanya
kazi ya kuchimba jasi (gypsum) lakini changamoto kubwa kwetu ni soko.
Wanakijiji wanachimba jasi nyingi kuliko uwezo wa kiwanda,” alisema.
Wakati huo huo, Waziri
Mkuu amepokea mchango wa sh. milioni moja kutoka Mkurugenzi wa Kampuni
ya Premalt Limited, Bw. Anand Chandra zikiwa ni mchango wao kwa ajili ya
wakazi wa Bukoba walioathirika kwa tetemeko la ardhi lilitokea Septemba
10, mwaka huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, OKTOBA 3, 2016


