Breaking News

Walioshirikiana na mkandarasi aliyejenga jengo la kituo cha afya cha Kabyaile Kagera kukamatwa.




Mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali mstaafu Salum Mstapha Kijuu ameagiza watafutwe na wakamatwe watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Misenyi walioshirikiana na mkandarasi aliyejenga jengo la kituo cha afya cha kijiji cha Kabyaile ambacho kiliathirika na tetemeko la ardhi lilitokea mkoani humo kutokana na sababu ya kujengwa chini ya kiwango ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo baada ya kubaini udanganyifu uliofanywa na mkandarasi anayemiliki kampuni ya Cosmas aliyejenga kituo hicho kilichoko kwenye eneo ambalo yanafanyika maandalizi ya ujenzi wa  kituo cha afya cha kata ya Ishozi kilichoathirika na tetemeko la ardhi aliyetumia udongo katika kuunganisha tofali na kufunika udongo huo kwa sementi kidogo, ameeleza ujenzi huo hauendi sambamba na viwango vya ujenzi wa nyumba za serikali na ndio maana kituo hicho kiliathirika na tetemeko.

Meja Jenerali mstaafu huyo pia amekagua maandalizi ya ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Ishozi unaofanywa na askari wa jeshi la wananchi wa Tanzania kikosi cha makao makuu na kuwahimiza kumaliza kazi hiyo haraka amewahimiza wananchi waendelee na mchakato wa kujenga nyumba zao za makazi, naye meja Burchard Kakula mkuu wa kikosi cha kijeshi amesema anao uhakika kazi itamalizika kwa wakati, huku Christma Richard akieleza changamoto ambazo wananchi wanazipata kwa sasa zinazochangiwa na ukosefu wa kituo cha afya.