
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN leo tarehe 1-Oct-2016
ameongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam katika uzinduzi rasmi wa
kampeni ya upandaji miti inayojulikana kama Mti wangu Jijini Dar es Salaam.
Akihutubia
mamia ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo katika eneo la barabara ya
Kilwa – Kurasini katika wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais
ameviagiza vyombo vya dola mkoani Dar es Salaam ambavyo vimepewa jukumu
la kutunza miti hiyo iliyopandwa ili isiharibiwe vihakikishe vinatekeleze
jukumu ili kikamilifu ili kuhakikisha miti hiyo iliyopandwa inakuwa vizuri ili
kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa miongoni mwa Majiji bora katika utunzaji
wa Manzingira.
Makamu
wa Rais SAMIA SULUHU HASSAN amesisitiza kuwa kampeni hiyo ambayo ameizindua
Jijini Dar es Salaam inatakiwa ifanyike nchini kote kama hatua ya kurejesha
uoto wa asili na utunzaji wa vyanzo vya maji kote nchini.
Amesema
kuwa jitihada za kupanda miti nchini zinatakiwa kuimarishwa maradufu kwani
zitasaidia katika uhifadhi wa mazingira hususani katika suala zima la kupambana
na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Makamu
wa Rais katika hotuba yake ameeleza kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha
kuongezeka hewa ya ukaa katika jiji la Dar es Salaam kutokana na ongezeko la
viwanda na idadi kuwa ya watu hivyo jitihada za pamoja kati ya serikali,taasisi
binafsi,asasi za kiraia na wananchi zinahitajika katika kutunza mazingira na
kupanda miti.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pia amepongeza
jitihada za uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam katika uboreshaji na uimarishaji
wa mifumo ya maji katika barabara itakayosaidia kurahisisha umwagiliaji wa miti
iliyopandwa.

Amesema
anafaraja na matumaini makubwa kuwa kampeni aliyoizindua ya upandaji miti
itakuwa endelevu na miaka michache ijayo italifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa
kivutio na mfano wa kuigwa na mikoa mingine kwa kuwa na mwonekano mpya na wa
kuvutia.
Baada
ya kuzindua kampeni hiyo jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais ambaye
aliambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu Rais Mazingira na Muungano
January Makamba na Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe
alifanya ziara fupi ya kutembelea na kukagua mifumo wa maji katika barabara ya
Nyerere na Ally Hassan Mwinyi itakayotumika kumwagilia miti iliyopandwa pamoja
na kuongeza na wananchi walioshiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la
Gymkana.
Imetolewa
na
Ofisi
ya Makamu wa Rais
Dar
es Salaam
1-Oct-16.