Breaking News

Kiongozi wa vyama vya upinzani nchini Kenya, Raila Odinga aiwakilisha serikali nchini India

Kiongozi mkubwa wa umoja wa vyama vya upinzani nchini Kenya (NASA), Raila Odinga amefanya ziara ya kuiwakilisha serikali ya Kenya nchini India.
Odinga katikati akiwa na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi
Odinga ambaye ameongozana na Mkewe, Mama Ida Odinga mapema leo wakiwa jijini New Delhi wamekutana na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi na kujadili mambo kadha wa kadha ya kimaendeleo baina ya nchi hizo mbili.
Mimi na mke wangu Ida Odinga tumefurahi kupokelewa na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, Kenye na India zimekuwa na urafiki wenye manufaa kwenye sekta mbalimbali kwa miongo mingi na ni imani yangu kuwa ziara hii itakuwa yenye manufaa kwa mataifa yote mawili.“ameandika Raila Odinga kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Kwa upande mwingine Odinga amesema kuwa wamejadili ongezeko la wawekezaji kutoka India katika Sekta za afya nchini Kenya na jinsi ya kuimarisha usafiri wa majini baina ya mataifa hayo.
Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa na baadhi ya wafuasi wa NASA ambao wanahoji kiongozi huyo ameenda India kama nani? ile hali hana nafasi yoyote kwenye serikali nchini Kenya ambayo inaongozwa na hasimu wake Uhuru Kenyatta.
Mkanganyiko huo pia umeenda mbali zaidi kuwa Rais Kenyatta tangu waelewane na Raila Odinga amekuwa hamtumii Makamu wake wa Rais, Wiliam Ruto kwenye baadhi ya mikutano mikubwa ya kimataifa na ziara muhimu za kikazi.
Odinga amewasili nchini India tangu wiki iliyopita na anatarajiwa kurudi Kenya wiki hii huku kukiwa na tetesi kuwa kiongozi huyo na Uhuru Kenyatta watampokea Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwenye ziara yake nchini Kenya inayotarajiwa kuanza Ijumaa hii.