Breaking News

Kuwasweka ndani viongozi wa Chadema ni tishio kwa demokrasia – Mhe. Zitto

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe amedai kitendo cha viongozi wa juu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuswekwa ndani Jumanne hii ni shambulio jingine kwa ustawi wa demokrasia nchini Tanzania.

Zitto ameyasema hayo muda mchache baada ya Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho kusomewa mashtaka 8 katika mahakama ya Kisutu kuhusiana na maandamano.
“Nilikuwapo mahakamani leo kuonyesha mshikamano kwa Viongozi wenzangu waliofikishwa mahakamani kwa kinachoitwa uchochezi. Nawaambia Watanzania Mfumo wa Demokrasia ya Vyama vingi nchini upo hatarini kubomolewa,” Zitto aliandika facebook.
Aliongeza, “Tangu tuanze siasa za vyama vingi nchini sijapata kuona tishio kubwa kama hili la kuwasweka ndani Viongozi theluthi 2 ya Viongozi wa Kitaifa wa Chama kikubwa Cha pili cha Siasa nchini. Jambo la kushangaza zaidi ni ukimya usio kifani wa wanachama wa Vyama vya Siasa vya upinzani nchini. Tukiendelea hivi, amini nawaambia, Demokrasia ya vyama vingi inafutwa,”
Chadema kimelaani vikali kukamatwa kwa viongozi wao: “Zimekua ni sarakasi dhidi ya upinzani. njama hizi dhidi viongozi wetu hatutaweza kuzinyamazia, tutaendelea kuzilaani na tunaangalia uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria” Afisa habari wa Chadema Tumaini Makene ameileza BBC.
Bwana Makene amesema viongozi wa Chadema ambao wamekuwa wakiripoti polisi kwa tarehe zilizokuwa zimepangwa, ilikuwa ni siku yao ya kufika kituo cha Polisi.


Posted by Baraka Nicholas Rubambula