Breaking News

WAKILI AMTETEA RAIS MAGUFULI KITENDO CHA KUMTEUA KATIBU WA BUNGE


Mwanasheria na wakili wa kujitegemea, Leonard Manyama, leo amejitokeza kumtetea Rais John Magufuli kwa hatua yake ya kuteua Katibu wa Bunge mpya akisema kitendo hicho kilifuata sheria.

Katibu huyo mpya wa Bunge, Steven Kigaigai, aliteuliwa Oktoba 7 mwaka huu na Rais Magufuli wakati anafanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri wiki iliyopita.


Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake jijini Dar, Manyama amesema rais hajavunja katiba katika uteuzi wake huo ambapo alisema kwamba anayo mamlaka ya kisheria ya kumteua katibu huyo miongoni mwa watu au watumishi wenye madaraka ya juu kinafasi na uzoefu kwa mujibu wa Ibara ya 87 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Manyama aliendeleza kusema kuwa ibara hiyo inajitosheleza na haitegemei sheria yoyote ya kuifafanua na ameliomba Bunge lipitie upya baadhi ya sheria ili kuondokana na utata kama huo.


“Kifungu cha Katiba cha 7(3) cha Sheria ya Utawala wa Bunge kinampa mipaka Rais juu ya uteuzi wa Katibu – kwamba ateuwe watu watatu ambao watachaguliwa, lakini katika Katiba anapewa mamlaka ya moja kwa moja ya uteuzi,” alisema Manyama.


Hata hivyo, Manyama amesema kuwa katika mwongozo wa kikatiba yapo maeneo ambayo utekelezaji wake unakuwa wa moja kwa moja kwa baadhi ya ibara ambazo hazihitaji sheria yotote ya kikatiba.