SAKATA LA KUPINGA UKOMO WA UMRI WA RAIS NCHINI UGANDA....MEYA WA JIJI LA KAMPALA AKAMATWA
Harakati za kupinga kuondolewa ukomo wa umri wa rais zimeendelea kuwa chungu kwa wapinzani baada ya viongozi kadhaa wa Forum for Democratic Change (FDC) akiwemo meya wa jiji Erias Lukwago kukamatwa.
Kiongozi mwingine aliyekamatwa kuhusiana na sakata hilo ni Katibu Mkuu wa Uhamasishaji wa FDC Ingrid Turinawe huku na nyumba za wabunge wawili ikiwemo ya Bobi Wine kulipuliwa na watu wasiojulikana.
Meya Lukwago amekamatwa na polisi nyumbani kwake Wakaliga, tarafa ya Rubaga na amepelekwa kusikojulikana. Polisi walizingira nyumba ya Lukwago na wakamzuia kuondoka.
Wakati akizungumza na waandishi mapema Jumanne Lukwago aliilaumu serikali kwa kuigeuza nyumba yake kuwa kambi ya jeshi na kwa kukiuka haki zake wakati akitetea katiba.
"Haya yote yanaonyesha kwamba Rais Yoweri Museveni anaogopa nguvu ya umma. Kamwe hatutamruhusu kuchezea katiba kwa sababu ni jukumu letu kama raia. Ni lazima tupambane na tabia hii ya kuponyoka makosa," alisema Lukwago.
Taarifa zinasema wiki iliyopita mabomu mawili ya kurushwa kwa mkono yalitupwa kwenye nyumba za Mbunge wa Rubaga Kaskazini Moses Kasibante saa moja tu baada ya kurejeshwa nyumbani na polisi waliokuwa wanamshikilia kituo cha Kibuli baada ya kukamatwa bungeni.
“Tumepokea taarifa kwamba mabomu yalirushwa kwenye nyumba za wabunge wawili Allan Ssewanya (Makindye Magharibi) na Robert Kyagulanyi (Kyaddondo Magharibi). Timu zetu zimeanza kuchunguza matukio hayo,” amesema msemaji wa polisi Asan Kasingye.
Bomu katika makazi ya Ssewanyana lilirushwa saa 7.20 usiku. “Watu wasiojulikana wamerusha bomu la mkono kwenye nyumba yangu,” alithibitisha Ssewanya kupitia Facebook.
Katika eneo la Magere, wilaya ya Wakiso, Kyagulanyi ambaye ni maarufu kwa jina la Bobi Wine amesema nyumba yake ilirushiwa mabomu matatu ambayo yalilipuka na kuvunja madirisha ya chumba cha kulala mtoto wake.