POLISI NCHINI KENYA YAZIMA MAANDAMANO YA UPINZANI
Maandamano ya muungano wa upinzani NASA, Kisumu, Oktoba 6, 2017.
Siku moja baada ya kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kutangaza kujiondoa katika kinyang'anyiro cha urais uliopangwa kufanyika Oktoba 26, wafuasi wa upinzani wamemiminika Jumatano hii katika mitaa ya miji mbalimbali nchini humo.
Waandamanji wanadai maafisa wa Tume ya uchaguzi IEBC wajiuzulu na kuteuliwe wengine wakiwashutumu kula njama na chama tawala cha Jubilee katika uchaguzi wa urais uliofutwa na Mahakama ya Juu nchini Kenya
Polisi nchini Kenya wamerusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa muungano wa upinzani ambao wamekuwa wakiandamana mjini Kisumu, magharibi mwa nchi hiyo.
Maandamano pia yamefanyika katika miji mingine mikuu ingawa hali imekuwa tulivu. Idadi ya waliojitokeza walikuwa wengi kuliko maandamano ya awali..
Muungano wa Nasa umekuwa ukifanya maandamano kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kushinikiza mageuzi katika Tume ya uchaguzi (IEBC) kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mpya.
Wakati huo huo Mahakama Kuu imeagiza kushirikishwa kwa mgombea wa Thirdway Alliance Dkt Ekuru Aukot kwenye uchaguzi huo.
Hata hivyo Muungano wa upinzani Nasa unataka uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku zisizozidi 90 na wagombea wateuliwe upya.


