KARAGWE:TANESCO YAKAMATA NGUZO ZA UMEME ZILIZOJENGWA KINYEMELA
Maofisa wa shirika la umeme tanzania (TANESCO) mkoani Kagera wamefanikiwa kukamata nguzo nne za umeme zilizokuwa zimejengwa kinyume na utaratibu na watu ambao kwa sasa wanatafutwa kwenye maeneo ya kijiji cha Nyaishozi kilichoko katika wilaya ya Karagwe huku zikiwa zimefungwa nyaya zenye urefu wa zaidi ya mita 300 zilizokuwa ziunganishe huduma ya umeme kinyemela kwa baadhi ya wananchi katika kijiji hicho.
Maofisa wa TANESCO wamefanikiwa kukamata nguzo hizo baada ya kuendesha operesheni maalumu ya kushtukiza ya siku mbili katika maeneo mbalimbali yaliyoko wilayani Karagwe iliyokuwa na lengo la kuwabaini wanaohujumu miundombinu ya shirika hilo iliyoongozwa na mhandisi mwandamizi wa shirika hilo katika mkoa wa Kagera Felix Olang'.
Akizungumza wakati wa operesheni hiyo Olang' amesema nguzo na vyaya zilizokamatwa zina chapa ya nembo ya mkandarasi anayejenga miundombinu ya mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA) unaotekelezwa katika wilaya hiyo ya Karagwe.
Kwa upande wake, afisa usalama wa shirika hilo katika mkoa wa Kagera Steven Maganga akizungumza amesema kujiunganishia umeme ni kinyume na taratibu na sheria hivyo ametoa onyo kwa wanaojihusisha na vitendo hivyo, naye mmoja wa maofisa kampuni ya ukandarasi anayosimamia mradi REA katika wilaya ya Karagwe Msami Ramadhani amekana kuwa kampuni hivyo hausiki na suala hilo.
#ITV-Tanzania