WALIMU WA SHULE YA MSINGI KIGONGONI WAJISAIDIA PORINI BAADA YA KUKOSA CHOO
Shule ya msingi Kigongoni iliyoko wilayani Monduli mkoani Arusha inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa choo unaosababisha wanafunzi zaidi ya elfu moja (1,000) kutumia matundu manne ya choo yenye hali mbaya ,huku walimu wakilazimika kupata huduma hiyo vichakani hali inayotishia usalama wa afya zao na wanafunzi wao.
Kufuatia hali hiyo benki ya(TPB) imetoa mchango wa milioni sita ambazo zimewezesha kujenga matundu 18 ya vyoo ,msaada ambao wanafunzi ,walimu na viongozi wa kamati ya shule pamoja na kushukuru wamesema umepunguza ukubwa wa tatizo na lakini bado mahitaji ni makubwa hasa kwa walimu.
Watendaji wa benki hiyo akiwemo mkurugenzi wa TEHAMA Bw. Jema Msuya na meneja wa TPB mkoa wa Arusha Bw. Ayubu Sapi Mkwawa wamesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu waliojiwekea wa kurudisha sehemu ya faida kwa wananchi.
Afisa elimu ya msingi wa wilaya ya Monduli Bi.Teresia Krara amesema asilimia kubwa ya shule za msingi bado zina mahitaji makubwa na pamoja na kuishukuru benk hiyo amewaomba wadau wengine wakiwemo wawekezaji, mashirika,taasisi na wananchi wenye uwezo kuona umuhimu wa kusaidia elimu.
Shule hiyo yenye walimu 22 ambayo pia inakabiliwa na tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu iko katika ukanda wa bonde la ufa ambalo asilimia kubwa ya wananchi ni wakulima wakubwa wa ndizi na mboga mboga na pia imezungukwa na hifadhi ya taifa ya ziwa Manyara.
#ITV