POLISI RUSSIA WASUMBUKA NA MATISHIO FEKI YA MABOMU
Polisi wa miji kadhaa mikubwa nchini Russia, ikiwemo Moscow, wamesumbuliwa na ripoti nyingi feki za matishio ya mabomu. Hadi sasa operesheni za kutafuta mabomu bado zinaendelea kwenye sehemu 190 za miji mikubwa 17 nchini humo.
Habari zinasema polisi wa mji wa Petropavlovsk wamepewa taarifa nyingi kwa njia ya simu kuhusu tishio la mabomu, na kutokana na taarifa hizo waliwaondoa watu kutoka shuleni, madukani na majengo ya serikali. Baadaye polisi katika miji kadhaa mingine pia walipata ripoti feki kama hizo.
Idara ya usalama ya Moscow imepata ripoti zaidi 100 za simu ndani ya saa kadhaa za mchana, zikidai kuwa magaidi wameweka mabomu katika sehemu nyingi za vituo vya treni, vyuo vikuu na maduka, na idara hiyo iliwaondoa watu karibu elfu 50 kutoka kwenye majengo mbalimibali, kabla ya ukaguzi kuthibitisha kuwa matishio hayo siyo ya kweli.
#CRI