Breaking News

MAOMBEZI YA TUNDU LISSU YAGONGA MWAMBA....POLISI WAPIGA MKWARA MZITO


Mkusanyiko wowote ambao unatarajiwa kufanyika kumuombea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, utakumbana na wakati mgumu kutoka vyombo vya dola.

Polisi imeshazuia mkusanyiko wa maombezi hayo uliokuwa umeandaliwa na Chadema mjini Sumbawanga kwa madai kwamba utasababisha uvunjifu wa amani.

Jana, Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) lilitangaza kufanya maombi kama hayo ya Sumbawanga kesho jijini Dar es Salaam huku likiwaalika viongozi mbalimbali wa dini lakini kabla siku yenyewe haijafika, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ameyazuia na kutangaza kutoruhusu mkusanyiko wowote wenye nia ya kumuombea mtu fulani.

Awali, Bavicha ilisisitiza kwamba haitarajii kuona maombi hayo yakizuiliwa kwa sababu hawaendi kufanya siasa, bali maombi kwa ajili ya Lissu na viongozi wengine wa Taifa kama ambavyo wamekuwa wakitoa wito wa kuombewa.

Maombi ya Bavicha yamepangwa kufanyika katika viwanja vya TIP, Sinza na tayari viongozi mbalimbali wa Kiislamu na Kikristo wamealikwa kwa ajili ya kuongoza maombi hayo.

Makamu Mwenyekiti wa Bavicha (Tanzania Bara), Patrick Ole Sosopi aliwaambia wanahabari jana katika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam kuwa, “Sisi tumeratibu tu maombi haya lakini hatutazungunza chochote, tutawaacha viongozi wa dini waongoze maombi hayo.”

Ole Sosopi alisema wametuma barua ya mwaliko kwa taasisi mbalimbali za dini ikiwamo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na kwamba wanasubiri majibu.

“Tumetoa taarifa pia kwa jeshi la polisi kama sheria inavyotaka. Hatutarajii kuzuiwa kwa sababu tumefuata taratibu zote kama sheria inavyotaka. Mmiliki wa uwanja amekubali, Serikali ya mtaa pia imeridhia jambo hilo,” alisema Ole Sosopi na kusisitiza “Hili jambo ni la kitaifa, tutalifanya kwa amani na utulivu mkubwa.”

Alisema ikitokea kuzuiwa, jeshi la polisi litoe sababu za msingi kwa nini wanawanyima wananchi haki yao ya kufanya maombi.

“Viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwamo Rais John Magufuli wamekuwa wakiwataka wananchi wawaombee, nasi katika maombi haya tutakwenda kumwombea ndugu yetu Lissu pamoja na viongozi wengine kwa ujumla,” alisema Ole Sosopi.

Ni kama Ole Sosopi alikuwa anajua kile ambacho kingefuata kwani baadaye Kamanda Mambosasa aliitisha mkutano na wanahabari akisema suala la maombi halijanza leo wala jana hivyo wakazi wa kanda maalumu (Dar es Salaam) lazima wafuate utaratibu.

“Hivi mtu anatoka Kimara, mwingine Mwenge halafu mnakutana sehemu kisha mnakwenda kufanya maombi Msimbazi! Haya hayatakuwa maombi, bali maandamano na hatutayaruhusu na wakithubutu kufanya hawatazidi hatua tano, wataangukia mikononi mwa polisi,” alisema.

“Ukiwa kanisani wewe fanya maombi hata usiku kuchwa hatutashughulika na wewe.”

Kamanda Mambosasa alisema maombi yanafanyika katika sehemu maalumu lakini kitendo cha watu kujikusanya sehemu moja kisha kuanza safari ya kwenda kufanya maombi mahali fulani siyo sahihi na ni kutotii sheria zilizopo.