Breaking News

WATENDAJI WA KUJITOLEA WASIMAMISHWA KAZI WILAYANI HANDENI


Mkuu wa Wilaya ya Handeni ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani hapo, Godwin Gondwe ameagiza kusimamishwa kazi watendaji wa kujitolea wakidaiwa kuhujumu mali za Serikali.

Gondwe ametoa agizo hilo jana katika Kijiji cha Kwankonje, Kata ya Magamba ndani ya msitu wa Kwapanga akiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama walipoenda kuangalia uharibifu uliofanywa na wananchi.

Zaidi ya hekta 300 zimevunwa mkaa na mbao.
Amesema watendaji wa kujitolea wasimamishwe kazi kwa kuwa asilimia kubwa wanashindwa kusimamia kazi na kuisababishia Serikali hasara huku akitoa mfano wa kijiji hicho ambacho msitu wa hifadhi umevunwa huku wao wakiwapo.

Mkuu wa wilaya amesema wapo maofisa ugani, afya, waratibu wa elimu na watumishi wengine wa Serikali wanaopaswa kukaimishwa nafasi za watendaji kwa muda wakati halmashauri ikisubiri kuajiri.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, William Makufwe amesema analifanyia kazi suala hilo, hivyo watendaji wote ambao wamefanya makosa watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Amesema halmashauri ina vijiji 91 ila watendaji wa kuajiriwa waliopo ni 31, hivyo ni vigumu kuwaondoa wote ila kwa masuala ya kukiuka mikataba ya kazi wale wote waliosababisha hasara kwa Serikali lazima wachukuliwe hatua.

Ofisa misitu Wilaya ya Handeni, Elinihaki Mdee amesema msitu huo unaharibiwa na wananchi kwa asilimia 85 kwa kuwa wamekata miti mikubwa.

Mohamedi Mwikalo mkazi wa kijijji cha Kwamsundi amesema biashara hiyo sio ya wananchi peke yao wapo viongozi wakubwa wa kata pia wanahusika ambao wanawateja wao kutoka Dar es Salaam na Zanzibar ambako ndio kuna soko kubwa la mkaa na mbao hivyo kumuomba mkuu wa wilaya kuongeza nguvu kupambana na watu hao.