Breaking News

POLISI WAPIGA CHINI MAANDAMANO YA BAVICHA KILIMANJARO



Baraza la  Vijana la Chadema(Bavicha), wamesema wanatarajia kufanya maandamano ya amani yenye lengo la kuipongeza kambi rasmi ya upinzani bungeni.

Akizungumza jana Jumatatu katika mahafali ya Umoja wa Wanachama wa Chadema Vyuo Vikuu (CHASO), Mkoa wa Kilimanjaro, Katibu Mwenezi wa Bavicha, Edward Simbeyi alisema kuwa watafanya maandamano mapema mwezi huu ili kuipongeza kambi hiyo ambapo amesema imekuwa ikipigania rasilimali za nchi.

Simbeyi ambaye ni mratibu wa CHASO taifa,alisema wanakusudia kufanya hivyo kama chama cha CCM  kilivyofanya maandamano ya kumpongeza Rais Magufuli kwa kuzuia mchanga wa madini (Makinikia).

Alisema kuwa wabunge wa upinzani wamekuwa wakipambana kwa kujenga hoja  bungeni kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao wenyewe badala ya watu wachache kunufaika.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema kuwa maandamano yalishapigwa marufuku na  hayaruhusiwi kufanyika mahali popote.

“Kama walijitokeza watu wakitaka kufanya maandamano ya kumpongeza Rais wakazuiliwa na wao pia wasijaribu kufanya hivyo,”alisema Issah.