Breaking News

LOWASSA AWAFUNDA WAKENYA KUHUSU UCHAGUZI MKUU UJAO

 Wakati Uchaguzi Mkuu wa Kenya ukitarajiwa kufanyika Agosti 8,2017, Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Lowassa na Rais Uhuru Kenyata wa nchi hiyo, wamewahadharisha Wakenya.

Akizungumza jana katika shughuli za mazishi ya aliyekuwa Waziri wa usalama nchini Kenya, Jenerali Mstaafu, Joseph Nkaissery aliyefariki hivi karibuni baada ya kuugua ghafla yaliyofanyika katika Jimbo la Kajiado, Lowassa alisema vurugu hizo ziliwatia aibu Wakenya.

“Mmetoka kwenye mapigano juzi ya kikabila yaliyotia aibu, naombeni msirudi huko, naombeni msirudi huko. Nchi yenu nzuri, ninyi wamoja, mmepata maendeleo ya kutisha. Tunastahili kuwaoneeni wivu, tunawaambia endeleeni,” alisema Lowassa na kuongeza: “Sasa mmepata uzoefu wa uchaguzi uliokuwa na fujo na matokeo yake. Lakini nawasifu Wakenya baada ya maridhiano mmeungana, mmeongoza nchi mmepata maendeleo. Nawapongeza sana.”

“Amani hii ndugu zangu Wakenya ndiyo inayowaleeteeni mambo yote mliyonayo. Ninyi hamjui, mimi nasikiliza sana TV ya Nipashe kuangalia mambo ya Kenya. Wakenya mnajilaumu, lakini ninyi mko mbele sana kimaendeleo kuliko nchi nyingine za Afrika Mashariki. Ninyi si watu wa kujilaumu, ni watu wa kujivuna,” alisema.

Naye rais Uhuru aliwataka Wakenya kufuata mfano wa Jenerali Nkaisery kwa kuhubiri amani.

“Kwanza katika wakati huu ambao tumebakiza siku chache kwenda kwenye uchaguzi, nawaomba Wakenya tuchukue mfano wa ndugu yetu Joseph. Jamani tuwe na amani, tuhubiri amani, tupendane. Tukijua kwamba uchaguzi waja lakini Kenya itabaki wakati wa uchaguzi.

“Kila mtu awe na uhuru wa kuomba kura yake na siku ya kupiga kura upande alipo, turudi nyumba tungojee matokeo, Kenya isonge mbele,” alisema Rais Kenyatta.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliyemwakilisha Rais John Magufuli alisema Kenya imempoteza mtu muhimu aliyekuwa akishughulikia amani ya Afrika Mashariki. “Tanzania haiwezi kuwa salama kama Kenya haitakuwa salama,” alisema.
#Mwananchi