Breaking News

SPIKA WA BUNGE ATOA POVU BAADA YA WABUNGE KUSUSIA FUTARI ALIYOIANDAA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Job Ndugai amewakumbusha wabunge wa vyama vya upinzani hasa vinavyounda UKAWA umuhimu wa jamii kukaa pamoja, kujadiliana na kumaliza tofauti zao.

Ndugai ambaye ni mmoja wa wabunge wa Bunge la 11 aliyasema hayo baada ya baadhi ya wabunge hasa wa upinzani kususia futari aliyoiandaa siku ya Jumanne kwa ajili ya wabunge wote. Kiongozi huyo wa juu wa mhimili huo alisema kuwa licha ya jukumu zito la kujadili na kupitisha bajeti ya serikali ya 2017/2018, ushirikiano kwa jamii ni muhimu.

Jambo hilo lilmfanya asiwe na raha na kuamua kuzungumzia ndani ya bunge kwa upole kabisa ambapo alisema kuwa, baada ya kuhudhuria futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu Jumatatu, na baada ya kuwepo tetesi za kususia ya kwake alisema, amejifunza kuwa baadhi wamekatazana kuhudhuria shughuli kama hizo.

“Lakini nikajifunza kitu kimoja ambacho sikupenda kukisema, ila nikiseme hapa kidogo. Kuna wenzetu wamekatazana rasmi kuhudhuria shughuli kama hizi.”

Ndugai aliyasema hayo Jumanne wakati akihitimisha kipindi cha maswali na majibu kabla ya kupisha mapumziko na kisha kupigiwa kura kwa bajeti ya serikali.

"Bunge linaendeshwa kwa mawasiliano ya namna mbalimbali baina ya wabunge na uongozi.  Endapo kuna jambo linakwaza na kusababisha watu wasipate futari pamoja,  ni vizuri wakae pamoja na kuondoa jambo hilo," alizungumza Ndugai.

Licha ya kutoa tahadhari hiyo, Ndugai alisema kuwa wabunge hao wana uhuru wa kufanya hivyo (kutohudhuria) kama wanaona ni sawasawa.

“Siyo mwezi wa chuki na kubaguana. Niwakaribishe tena kwenye futari kwa watakaoweza kufika. Watakaoshindwa In Sha Allah, kila la heri. Tutaendelea kuwa pamoja mjengo huu huu,” alisema Spika Ndugai akihitimisha nasaha zake.