CHADEMA WATOA NENO KUHUSU MNYIKA KUBEBWA JUU JUU NA ASKARI WA BUNGE

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Ubungo kimesema
kitendo cha Mbunge wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika kutolewa kwa nguvu
Bungeni Juni 2, si cha kiungwana.
Akizungumza leo (Jumapili), Juni 4, Katibu Mwenezi wa Chadema, Ubungo,
Perfect Mwasiwelwa amesema Wapinzani akiwamo na Mnyika wamekuwa watetezi
wa masuala ya madini kwa miaka takribani 20 ila sasa wanaonekana sio
wazalendo wa Taifa lao.
"Kitendo cha Mnyika kubebwa mzobemzobe na kutupwa nje ya mlango wa bunge
na ukiangalia mazingira alitaka kudondoka, kwa kweli ni kitendo cha
kinyama, sio cha kiungwana, sio cha kibinadamu na Kitanzania kabisa,"
amesema Mwasiwelwa.
Amesema kuwa Chadema inapinga matumizi ya nguvu kwa ajili ya kuzima
upinzani kupigania suala la madini kama ilivyofanyika kwa Mnyika ambaye
ni Waziri kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini.


