ZILIZOTUFIKIA:RAIS MAGUFULI AVUNJA BODI YA WAKALA WA UKAGUZI WA MADINI (TMAA)
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ameivunja
Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na pia kumsimamisha
kazi Mkurugenzi Mtendaji wake kwa kushindwa kusimamia vyema sekta ya
madini.
Mbali
na kuchukua hatua hiyo, Rais Magufuli ameviagiza vyombo husika pia
kuwachukulia hatua watendaji wa TMAA na Wizara ya Nishati na Madini
waliohusika kuisababishia hasara serikali kutokana na mchanga wa madini
uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje.
Rais
Magufuli ametoa kauli hiyo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati
alipokuwa akipokea taarifa kuhusu ripoti ya ukaguzi wa mchanga wa madini
wa makontena 277 yaliyozuiliwa bandarini.
“Bodi
ya TMAA nimeivunja kuanzia leo. Mkurugenzi Mtendaji wa TMAA anasimama
kazi kuanzia leo lakini vyombo vya dola ambavyo vipo hapa muanze
kuwafuatilia wafanyakazi wa TMAA waliohusika na mlolongo wote ili hatua
za kisheria zianze kuchukuliwa” alisema Rais Dkt Magufuli.
Lakini
wakati huo huo Rais Magufuli ameikosoa Wizara ya Nishati na Madini kwa
kushindwa kuisimamia vizuri TMAA ambayo ipo chini yake, na hivyo
kuisababishia serikali hasara kubwa kutokana na usafirishwaji wa mchanga
nje ya nchi.