TRUMP AIMWAGIA TANZANIA MABILIONI YA PESA KUKABILIANA NA UKIMWI
Marekani imetangaza kuipatia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ufadhili wa kukabiliana na virusi vya ukimwi.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Serikali ya Marekani kupitia ofisi ya Rais
Donald Trump imeeleza kuwa imeipa Tanzania kitita cha dola milioni 526
kutoka mfuko wa PEPFAR, ili kufanikisha mpango wa kutoa huduma kwa zaidi
ya watu milioni 1.2 wanaoishi na virusi hivyo.
Mwakilishi wa ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Virginia Blaser
amesema kuwa wanalenga kufanikisha kizazi kilicho huru kutoka virusi
nchini Tanzania. ”Kwa niaba ya raia wa Marekani, tunafurahia ushirikiano
wetu na Tanzania na tunajitahidi kuhakikisha hakuna anyeachwa nje,”
Amesema.
Ufadhili huo umelenga matibabu, ukaguzi, na kuzuia maambukizi mapya ya
virusi hivyo kuanzia sasa hadi Septemba mwaka ujao, pia fedha hizo
zitatumika kuimarisha maisha ya wajane na mayatima wa viurusi hivyo,
kuzuia dhulma za kijinsia, pamoja na kuwafikia zaidi ya watu laki tatu
walioambukizwa.
Aidha, Serikali ya Marekani itashirikiana na Serikali ya Tanzania
kutekeleza huduma za kuwapima raia milioni 8.6 ili kuwawezesha kujua
hali yao ya virusi, imeeleza taarifa hiyo ya BBC.
Fedha hizo zitapitia katika mashirika mbalimbali yanayoendesha miradi ya
afya nchini Tanzania, kama vile (TACAIDS), na Benjamin Mkapa (Benjamin
Mkapa HIV/AIDS Foundation (BMAF)) yanatarajiwa kushiriki kufanikisha
mpango huo.
Marekani ilikatiza ufadhili wake wa miradi kama hiyo nchini Kenya pamoja
na kuyazuia mashirika dhidi ya kufanikisha miradi yoyote na wizara ya
afya ya taifa hilo kutokana na usimamizi mbaya wa fedha.