Prof Maghembe Awashukuru Waliovamia Hifadhi za Misitu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amewashukuru
wavamizi wa Msitu wa Hifadhi wa Isawima wilayani Kaliua ambao wameamua
kwa hiari yao kubomoa makazi na kuondoka wao na mifugo yao katika eneo
hilo ambalo ni miongoni mwa vyanzo vya maji ya Ziwa Tanganyika
.
Ameyasema hayo Wilayani Kaliua mara baada ya kusomewa taarifa ya
utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa Wavamizi hao katika Msitu wa Hifadhi
na kutembelea eneo walipoondolewa wavamizi na kisha kupata fursa ya
kuongea na wananchi.
Amesema kuwa Serikali imefurahishwa na uamuzi huo uliochukuliwa na watu
hao baada ya kupata elimu kuhusu athari za kimazingira za wao
kung’ang’ania kuendelea kuishi katika maeneo yaliyohifadhiwa na kuamua
kuondoka bila kushurutishwa.
“Serikali haina shida ya kumuonea mtu na ndio maana tumekuwa tukiitumia
zaidi elimu jambo ambalo limeleta mafaniko makubwa katika eneo la
Hifadhi hii ambapo zaidi ya asilimia ya 70 ya watu waliokuwa wamevamia
wameondoka,”amesema Prof. Maghembe