Waziri Nchemba Awaonya Wanaotumia Dini Kufanya Uhalifu
Waziri
wa Mambo ya Ndani Tanzania Mwigulu Nchemba, amewaonya waumini wa dini
mbalimbali nchini kutotumia mwamvuli wa dini kufanya vitendo vya uhalifu
ikiwemo kudhuru maisha ya wengine, huku akitangaza kulegeza masharti ya
usajili wa nyumba za ibada
Waziri
Mwigulu ametoa onyo hilo jana alipokuwa mgeni rasmi katika tamasha la
Pasaka lililofanyika katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam,
ambapo alisema serikali haitawavumilia watu wa aina hiyo.
Katika
hotuba yake fupi Waziri Mwigulu alisema serikali inatambua uhuru wa
kuabudu iliyoutoa kwa wananchi wake na inaunga mkono kazi nzuri
inayofanyika kupitia ibada, lakini uhuru huo usikwaze wengine, na wala
usivunje sheria.
Alisema
"Ucha Mungu Siyo Udini", hivyo ni sahihi kwa waumini kumcha Mungu kwa
kiwango wanachopenda lakini si kuwashikia silaha watu wengine ili
wajiunge na dini zao.
“Wale
ambao watatumia misimamo iliyopitiliza kudhuru maisha ya watu wengine,
serikali itasimama na kuwahesabia kuwa ni waovu na tutashughulika nao
kama wahalifu wengine” Alisema Mwigulu
Katika
hatua nyingine, Waziri Nchemba ameagiza taasisi zilizo chini ya wizara
yake kulegeza masharti ya usajili wa nyumba za ibada, badala ya kuwapa
njia ngumu kwani nyumba hizo ni muhimu kwa ajili ya kumuombea Rais
Magufuli na taifa kwa ujumla
"Nimeelekeza
watu wangu kuwa waelekezeni watu wanaotaka kusajili nyumba za ibada
watimize masharti na muwasajili, hatuwezi kuweka masharti magumu ya
kusajili nyumba za ibada halafu tukaweka masharti rahisi ya kusajili bar
na kumbi za disco" Alisisitiza Mwigulu
Aliwataka
waumini wa dini mbalimbali kuendelea kuliombea taifa, huku akiwapongeza
kwa kazi nzuri ya maombi waliyoifanya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015.
"Endeleeni
kuliombea taifa letu, wana maombi mkishaomba, mambo yakawa mema, watu
huwa hawakumbuki kama mlisugua magoti… hata wakati wa uchaguzi mliomba
ndiyo maana tukapita salama wakati kuna watu walitaka kuona Tanzania
inayojidai kuwa na amani, itakuwaje.....
"..Wakati
ule walikuwa wameandaa magari ya washawasha na mabomu ya machozi lakini
nilipofika wizarani nilikuta yale magari yapo hayakutumika pamoja na
mabomu, kazi mlishamaliza wana maombi"
Waziri
Mwigulu pia alitumia nafasi hiyo kuwahakikishia wasanii wa nyimbo za
injili kuwa serikali itafanya kila iwezalo kulinda maslahi ya kazi zao,
huku akipongeza kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli ya kuwaletea
maendeleo wananchi licha ya kupingwa na baadhi ya watu na kutolea mifano
ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa ndege, elimu bure na mengine.