Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Yalaani Mauaji ya Askari Polisi 8 Mkoani Pwani
Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imepokea kwa masikitiko
taarifa ya kuuwawa kwa askari wanane (8) wa Jeshi la Polisi, katika
tukio lililotekelezwa na watu wasiofahamika jioni ya Aprili 13, 2017
katika kijiji cha Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inalaani vikali mauaji haya ya
kikatili ya askari polisi waliokuwa kazini na wasiokuwa na hatia. Aidha,
tunaungana na Watanzania wengine kuwapa pole familia za wafiwa na Jeshi
la Polisi kwa ujumla.
Kumbukumbu
zinaonyesha kuwa matukio ya mauaji ya askari polisi na wananchi wengine
maeneo tofauti Mkoani Pwani tangu mwaka 2015 yamekuwa yakiongezeka na
kusababisha uvunjifu wa haki za binadamu, hususan haki ya uhai
inayolindwa na Katiba ya nchi, na madhara mengine kwa familia za
wahanga, kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Haki
ya kuishi kama zilivyo haki nyingine, inalindwa kisheria, na pia
inalindwa na mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambayo Tanzania
imeridhia. Hakuna mtu anayepaswa kuporwa haki hii ya msingi kiholela.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) Ibara ya
14, kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi
ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.
Ikumbukwe
kwamba askari polisi wanapokuwa kazini wanatekeleza majukumu muhimu ya
kulinda raia na mali zao, kwa hiyo usalama wao unategemewa na Watanzania
wote. Yeyote yule anayewaua askari polisi siyo tu anataka
kuwachonganisha askari polisi na raia, bali pia anawaweka raia hao
katika hofu kubwa ya usalama wao na mali zao.
Hivyo basi, kwa mara nyingine, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inashauri kwamba:
1.
Katika kuhakikisha kuwa haki ya kuishi ya askari polisi na wananchi
wote inalindwa, Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla wafanye uchunguzi
wa kina ili kubaini sababu za mauaji haya kutokea kwa kujirudia Mkoani
Pwani, na kuhakikisha wahusika wote wanapatikana na wanafikishwa kwenye
vyombo vya sheria, ili sheria ichukue mkondo wake.
2.
Tume inawakumbusha wananchi kuwa vitendo vya ukatili, mauaji, na
matendo yote yanayokiuka Sheria yanayofanywa na raia wasio wema ni
ukiukwaji wa Sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala wa sheira;
Hivyo Tume inakemea matendo haya na kutaka yapigwe vita.
3.
Aidha, inawataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika
kuhakikisha upelelezi wa matukio hayo unakamilika ili hatua za kisheria
zichukuliwe kwa watakaobainika kuhusika na matukio haya.
Imetolewa na:
Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Aprili 14, 2017