Marekani Yadai Haina Muda wa Ziada wa Kuvumilia Vitisho vya Korea Kaskazini.
Mshauri
wa Rais Donald Trump wa masuala ya usalama, Herbert Raymond McMaster
amesema kuwa Marekani na China zinaelekea kupoteza uvumilivu dhidi ya
Korea Kaskazini inayoendelea na vitisho vya silaha za Nyuklia.
McMaster amesema makubaliano yanayojitokeza dhidi ya tabia ya vitisho vya Korea Kaskazini kwa sasa yanaijumuisha China.
Amesema
kuwa kuna makubaliano ya kimataifa, ikiwemo China kuhakikisha tabia hii
haiendelei, kwani kumekuwa na majaribio ya makombora ya hivi karibuni
yanayoonyesha tabia ya vitisho ya Korea Kaskazini hali ambayo
hawataivumilia zaidi.
Amesema
kuwa Rais Trump ameweka wazi kuwa Marekani na washirika wake
hawatokubali kuona utawala wa vitisho dhidi ya silaha za nyuklia.
Korea
Kaskazini imefanya jaribio la uzinduzi wa makombora ya masafa ya mbali,
hata hivyo lilikwama, ambapo Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence
amefika Korea Kusini saa chache baada ya jaribio hilo.
Akizungumza
katika kambi ya jeshi, Pence amesema anawahakikishia kuwa chini ya
uongozi wa Rais Trump ushirika wa Marekani na Korea Kusini haujawahi kuwa
na nguvu lakini kwa msaada wa jeshi hilo na Mungu uhuru utaendelea
kuimarika katika rasi ya Korea bila vitisho vyovyote.