Hatimaye 'Chura' wa Snura Mushi aruhusiwa kurukaruka kwenye Radio na TV
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye amemruhusu msanii wa muziki, Snura Anthony Mushi
‘Snura’ kuachia video yake mpya ya wimbo ‘Chura’ baada ya msanii huyo
kufanya marekebisho ya video ya wimbo huo na kukubaliwa na wizara.
Aidha, katika barua ya wizara imemtaka Snura kuomba radhi mbele ya
waandishi wa habari ili video hiyo ianze kuchezwa. Mapema mwaka huu
video ya wimbo huo ulitangazwa kufungiwa na serikali baada ya video hiyo
kukosa maadili ya kitanzania.
Akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa Maisha Basement
jijini Dar es salaam, Snura amesema anamshukuru Mh waziri Nape Moses
Nnauye kwa kumkubalia ombi lake la kuiruhusu kazi hiyo kutoka.
“Mh Nape ameuruhusu wimbo wangu mpya wa Chura na video Chura kupigwa
na kuonyeshwa katika vituo mbali mbali vya radio na runinga baada ya
kuona video yangu mpya ya wimbo ina maadili na ujumbe ndani yake ikiwa
ni kukidhi makubaliano ya awali kwamba wimbo wangu ‘Chura’ utafunguliwa
pale nitakapofanya video mpya ya muziki yenye maadili ya kitanzania,”
alisema Snura.
Aliongeza, “Video yangu mpya Chura inaeleza maana halisi ya neno
Chura. Chura ninayemzungumzia ni mwanamke anayeruka ruka katika
mahusiano kwa kubadilisha wanaume mbalimbali matokeo yake kupata
magonjwa sugu,”.
Pia katika barua hiyo ya Mh Waziri wa habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye amempa onyo kali msanii huyo kutokurudia kufanya
tena video zisiyokuwa na maadili ya kitanzania.


